Mwezi wa mfungo sita kwa karne kadhaa hivi sasa waislamu wamejizowesha hadi yakawazowea mapenzi yao ya kukumbuka uzawa wa Mtume Muhamad (S.A.W) na kwa ajili hiyo hufanya majumuiko ya kumsalia nakumtakia rehma, huku zikitajwa tarekh za mambo mbalimbali aliyoyatenda kwa kutanguliza uaminifu aliokuwa nao tokea utotoni,ujanani na zaidi tabia njema zisizo mfano.
Wengi wamemsifu, lakini kabla wanaadam kumsifu na kumsalia, Mola mwenyewe na Malaika wake na kuwataka waumini nao wamsalie na kumtakia rehma Bwana Mtume (S.A.W). Amesifiwa kuwa ni kigezo chema, tunahitajika kwenda katika mwendo wake ilitutimie katika uislamu wetu, pia tumekatazwa kwenda kinyume na Quraa’n na sunnah zake kwani anayezikengeuka Sunnah zake amesema hayuko pamoja nae.
Pamoja na sote kufurahia mazazi yake, ni wangapi fursa kama ya mwezi huu kuukumbuka uzawa wake kwa kuiga mwenendo wake? Ni waislam wangapi wanaomuunga mkono Mtume Muhamad (S.A.W) kikweli? Jee! Waislam wangeliipata wapi miongozo ya maisha yao na kujua uasili wao kama si kutokana na M/Mungu kumtuma Mtume Muhamad (S.A.W) kwetu kutufunza upweke wa Mola, ujira mkubwa wa malipo ya peponi na mateso makubwa yasiyo mfano kwenye mashimo ya motoni.
Ni yeye Sayydina Muhamad (S.A.W) ametufunza kwa ujumbe alioletewa na Mola wake. Mimi na wewe kwa mangapi tunamfuata mtukufu huyo wa daraja?
Katuonya tusilewe, nani analewa na yeye anajiita Muislam, jee! Yuko pamoja na Mtume huyo na kama hayupo naye anatarajia pepo huyo kwa kutegea aya za uwezo wa M/Mungu za kumsamehe mja makosa yote, nani ategeaye hilo baada ya kufanya jihadi ya nafsi yake na watu wake kuokoka na moto?
Yeye atakuwa zaidi ya nani wakati Mtume Muhamad (S.A.W) aliyesamehewa dhambi angali hai zilizotangulia na zitakazo kuja wakati wa uhai wake,bali aliomba msamaha daima kwa kumshukuru Muumba.
Ni nani huyo anayezini kisha anajinasibu kumpenda Mtume (S.A.W) ambaye ametukanya na dhambi hiyo kubwa? Kasomeshwa na nani tabia hiyo, ambaye eti anataraji Mtume amtakie shufaa?
Ni kina nani hao wanaofyeka mali za mayatima kisha wakajitaja ni vipenzi vya Mtume(S.A.W)asiefurahia hilo? Mtume akiyaogopa yale yote yanayomuudhi M/Mungu na alikuwa mwaminifu na mkarimu, mimi na wewe kwanini tusanzuwe mali yao kisha tujisifu ni vipenzi vya Mtume?
Ni wanawake gani hao wasiojistiri vile alivyoagiza Mtume halafu wapende Maulidi yake kisha wafanye ni jambo mbali na tafakuri na uongozi wake kwa waumini wakike na wakiume? Wamtegemee nani siku ya siku wakati wamesikia wake za Mtume walivyojistiri wakimkhofu Mola wao hawakuringia ukaribu wao na Mtume?
Ni wanandoa gani hao wanaotesana mke akamtolea mbovu mume na kutomtii na mume akamgeuza mkewe dampo la maudhi yake kwa machukizo na masimbulizi bila kuzingatia Mtume Muhamad (S.A.W) alivyoishi na wake zake? Ni wangapi walifukuza wake zao kwa kuwataliki na kuwavua kila chao tokea nguo hadi vyombo vya mikononi?
Ni Ulamaa na Sheikh yupi ambae hafanani na matendo yanayomstahikiya na huku akijua kuwa Ulamaa ni warithi wa Mitume.
Ni daktari yupi huyo ambae hutumia vijembe, mikasi na vidonge vyake kuziviza mimba kuficha ukweli wa haramu iliyopita kwa tamaa ya mapato wakati kipenzi chetu Mtume (S.A.W) hakufa na mali bali amali safi alizokuwanazo?
Ni kijana gani huyo wakiume alietoga akavaa herini akazungusha kidani shingoni na vikuku mkononi, jee! Afanane na nani wakati jinsia yake anaielewa, vipi huyu awe kipenzi cha Mtume wakati mwenyewe Mtume ameshaeleza jinsi mwanamume au mwanamke anaejifananiza na jinsia iliyotofauti naye kwa vivazi amelaaniwa na M/Mungu!
Ni nani huyo anaejipa ujabari akaitoa roho ya Muumini mwenziwe pasina sababu ya sharia anaemtaraji Mtume kuwa katika kundi la wema pamoja nae siku ya siku, wakati kila aliyemuuwa Muislamu muumini bila ya sababu ya sharia malipo yake ni Moto wa Jahanam milele?
Wangapi wamerejea kwa waliowaulia watu wao kuomba wawasamehe, wangapi waliolipa fidia ngamia 100, jee! hawapo walioliona hilo ni kosa kubwa? Vipi nao wajisifu wanampenda Mtume?
Basi haya na mengine mengi yawenimakumbusho kwa waumini ilitunaposema tunampenda tujifunze yeye alikuwa akiishi vipi, lipi hakuwa akilipenda lipi ameliamrishalitendwe, lipi amelikataza tuliwache? Sasa alokataza tuliwache tukalifanza tupo na nani Mtume (S.A.W) au sheytwan atayetuangamiza?.
Kumbuka na mimi nikumbuke, Mtume (S.A.W) ametanabahisha juu ya dalili za kiama kuna mambo yatayoanza kudhihiri nayo ni -:
1) Elimu ya dini itapuuzwa na kuwekwa kando.
2) Ujinga utazidi hususan katika masuala ya dini.
3) Kuingiliana katika mambo machafu kutadhihiri waziwazi.
4) Unywaji wa vilevi litakuwa jambo la kawaida.
5) Wanaume watapungua idadi yao, wanawake watazidi idadi yao hadi wanawake hamsini baadae watamuelekea mwanaume mmoja.
Basi tujifunze ili hiyo saa ikifika itukute tupo safi. Nani anataka saa imkutie klabu cha pombe?
Nani saa imkutie danguroni nani saa imkutie akiua wenziwe?
Nani saa imkutie anamsujudia Mola wake?
Nani saa imkutie anawahudumia wazazi wake na nani saa imkutie anatafuta elimu na ridhiki ya halali?
Hizo ni chaguzi kwetu kila mmoja.
Wako Mtiifu Muomba Maghafira
Al-Udii.

Lazima uwe mwanachama wa Zanzibarwebsite ili uweze kuweka ujumbe!
Join Zanzibarwebsite