بسم الله الرحمن الرحيم
الأسرة السعيدة - الوصايا العشر FAMILIA BORA- NYASIA KUMI UTANGULIZI: Familia ni taasisi ya kimalezi ya mwanzo ambapo muislamu anapata thamani na tabia zake. Kwa sababu hii familia ni kituo muhimu ambacho huupa nguvu umma, na jamii hupata mshikamano kwa kuwa hili ni tofali la mwanzo katika ujenzi wa jamii bora. Familia ndio kiungo cha kati baina ya mtu mmoja mmoja na jamii , na ikiwa nzuri huwa mzuri mtu mmoja mmoja kabla, na baadae jami ipia huwa nzuri. Na anaefuatilia kwa makini hali za familia zetu katika jamii yetu atagundua zimepatwa na maradhi mengi ambayo hapana budi kuyatibu na kujikinga nayo. Katika Matatizo ya familia zetu ni: 1: Kuongezeka idadi ya talaka katika ndoa mpya: Mara nyingi sababu huwa ni migongano iliyopo katika ujenzi wa ndoa yenyewe baina ya wanandoa. Kwa hiyo inahitajika kurejea katika misingi ya uislamu ili kuasisi mafunagamano na mahusiano bora baina ya wanandoa na kuziendeleza ndoa katika misingi salama iliyowekwa na dini yetu. 2:Kukosekano mawasiliano ya kutosha baina ya wanafamilia: Kwa kuwa mmoja kati ya wazazi wawili au wote wana mishughuliko mingi ya kutafuta rizki, ambapo wakati mwingi hupotea nje ya nyumbani. Kwa hiyo imekuwa sasa watoto wanapokea malezi kutoka kwa wenzao(wanawaiga), kutoka kwa mayaya (House girls), kwa walimu wa shule, televisheni na maintaneti. Hii imesababisha udhaifu mkubwa katika tabia za watoto wa kizazi cha sasa. Tatizo hili limezikuta nyumba nyingi sana isipokuwa zile ambazo Alla amezirehemu. 3: Kuyumba hali ya kiimani katika familia nyingi: Hakika hali ya kiimani kwa watu wa familia huathiri sana mafungamano ya kifamilia. Mahusiano baina ya wanandoa kwa hakika ni mahusiano ya kiimani yenye kudumisha upendo na rehma. Allah anasema: " وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجاً لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِي ذَلِكَ لآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ " (سورة الروم – 21) “Na katika ishara zake ni kukuumbieni nyinyi wake kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao, na amejaalia baina yenu mapenzi na huruma, hakika ishara zimo katika hayo kwa watu wanaotafakari.” Na imani huzidi na kupungua, huzidi kwa kumtii Allah na kushikamana na njia ya Allah. Na hupungua kwa kumuasi Allah na kuwa mbali na njia ya Allah (S.W). Ndio maana alikuwa mtu mmoja mwema akisema: إني لأعرف منزلتي عند ربي من خلق زوجتي و خلق دابتي . “ Hakika mimi najua nafasi yangu mbele za mola wangu kwa tabia za mke wangu na tabia za mnyama wangu” Yaani kuharibika kwa tabia za watu wa nyumbani kwangu ni ishara ya kuharika mahusiano yangu na Allah (S.W). Kwa hiyo kuzidi imani na kutulizana hali ya kiimani katika hali nzuri bila ya shaka ni nguzo muhimu ya maisha ya familia katika kuifanya bora. Kwa kuwa pamoja na misukosuko hii ya familia zetu , bado pia kuna tatizo la mikakati ya maadui wa uislamu kuzibomoa familia zetu, ni vizuri kueleza mbinu za kuzikinga familia zetu na matatizo haya. MAMBO KUMI YA KUFUATLIA ILI KUZIFANYA FAMILIA ZETU ZIWE NZURI: N.B: Kila familia ichukue katika mambo haya yale ambayo yananasibiana nayo na ambayo ina uwezo wa kuyatekeleza na kama itawezekana kuyafanyia kazi yote itakuwa ni bora na Allah ashukuriwe! 1: Kikao cha mazingatio ya Qur-an mara moja kwa kila wiki: Familia inakutana pamoja katika wakati wanaopatikana wote, kila mmoja atoe kipaumbele katika muda uliopangwa kwa ajili ya kikao hiki. Familia inasikiliza Qur-an kwa pamoja na kutafakari maana ya aya zinazosomwa kwa msaada wa anaeifahamu Qur-an miongoni mwao, la akikosekana basi hata kanda au CD. Kwa kufanya hivi familia itapata sakina (utulivu) na itafunikwa na rehama na itazungukwa na malaika, na Allak atawataja kwa wale walio mbele zake. Kisha wataondoka katika majlisi hayo hali wamesamehewa dhambi zao. 2: Kuhifadhi Qur-an: Tunashauri kuwa wakubaliane wote kuhifadhi aya moja kila siku. Na hii si ajabu ukakuta kila mmoja katika wanafamilia amehifadhi sehemu kubwa katika Qur-an hapo baadae kwa kutumia mbinu hii. Kilicho muhimu kuihifadhi aya na maana yake na kuusiana kuitekeleza kimatendo kwa jinsi inavyotutaka aya. 3: Kuhifadhi hadithi za Mtume (S.A.W): Chagueni hadithi mfano kutoka الأربعين النووية Kitabu cha hadithi 40 cha Imamu Nnawawiy na iandikwe ubaoni katika sehemu amabayo kila mtu ataiona. Na iachwe hapo kwa muda wa wiki moja kamili na isifutwe mpaka kila mtu ameihifadhi. 4: Kuwe na maktaba ya nyumbani: Kuwe na maktaba ndogo iliyo kusanya vitabu vya mustawa mbali mbali. 5: Kuendesha mashindano: Mashindano kwa watu wa familia hufanya nyoyo zipendane, nayo ni njia nyepesi ya kufikia kuyajua mambo kwa wepesi na kusahihisha ufahamu. Kwa mfano unaweza ukawasimulia kisa watoto na ukawashndanisha katika kukihifadhi, na si vibaya kuambatanisha mashindano na zawadi. 6: Kuwashirikisha watoto katika harakati za daawa na kijamii: Ni vizuri kuhudhuria msikitini katika swala za jamaa na watoto. Kuwasisitiza kuswali msikitini na kuwahi mapema kwa watoto wa kiume. Kwa watoto wa kike kuwahimiza kuswali mara tu wanaposikia adhana. 7: Kufunga funga za sunna: Kama kufunga jumatatu na Al-hamisi, siku tatu katika kila mwezi, mwezi 9 na 10 katika mfungo nne (Muharram), siku ya Arafa, siku sita za mfungo mosi (Shawwal) 8: Kufanya safari za kiibada: Kama Kwenda Makka, na msikiti wa Mtume Madina. 9: Kuwazoesha watoto mambo yafuatayo: Kukirimu wageni. Kuwafanyia wema majirani. Kuunga udugu. Kushiriki maziko na kusindikiza jeneza. Kutembelea wagonjwa. Kuchangia na kutoa sadaka katika shughuli za kijamii. Kutoa sadaka kila chenye manufaa kama nguo,pesa n.k. Kuwahimiza kusaidiana katika usafi wa nyumba, n.k 10; Kuwafatilia watoto katika kudumu na nyiradi: Nyiradi za asubuhi na jioni, na dhikri za hali kama kula na kulala, za kuingia nyumbani na kutoka, kuingia chooni n.k. Ndugu yangu haya ni baadhi tu katika mengi ambayo tunaweza kuyafanya ili kuhuisha familia zetu katika dini. Namuomba Allah atujaalie kizazi chema chenye kufata amri zake na kuacha makatazo yake.
|
© 2012 Created by zanzibarwebsite.com.
Lazima uwe mwanachama wa Zanzibarwebsite ili uweze kuweka ujumbe!
Join Zanzibarwebsite