NAPENDA PASI KIFANI       BUSHAKO NIMASHAKANI

NAPENDA  KIFUANI            NATEREMKIA  MAPAJANI

NAPENDA MI PUNGUANI      CHA MSINGI NAUMIYAA

NAPENDA UMBO LAKE         NYWELE ZAKE KADHALIKA

NAPENDA SAUTI YAKE        RANGI YAKE KUCHANGANYIKA

NAPENDA HARUFU YAKE      MANUKATO YAKE YANIWEWEZEKA

NAPENDA AKICHEKA           NINAPO  MFURAHISHA

NAPENDA AKIPEPESUKA      HADI NGUVU ZINAMUISHA

NAPENDA AKIWEWESEKA     ELIMU NIKIMFUNDISHA

NAPENDA NAPATA WAZIMU    NASEMA KWA UFASAHA

NAPENDA NAHISI KUZIMU      NA WALA SIFANYI MZAHA

NAPENDA  MUSINILAUMU       NAUGULIA   MAJERAHA

NAPENDA SISHAURIKI          NA  WALA SITAJUTA

NAPENDA HADI CHUKI         KWA KILA ANAYEMUITA

NAPENDA KIHAFUBEKI         ANIPITAE  NAMVUTA

NAPENDA  NA  SITAKI         WOTE WANAONIBEZA

NAPENDA WAKIHAMAKI       VIGAE  WAWEZA MEZA

NAPENDA WAKINISHTAKI     KUNIFUNGA MUNAWEZA

NAPENDA KIARABU         KISWAHILI NISHAPITA

NAPENDA MUHIBU          NA CHAKULA NISHAPIKA

NAPENDA SINA AIBU       BUSHAKO NIMESIKIKA.

Views: 79

Jibu Hii

Majibu ya Mjadala huu

Penda wangu upendavyo  Jua kuna mwisho wake

Vizuri uvionavyo              Mpambaji Mola wake

Leo tamu kesho ovyo       Huyo huyo utamke

UPO

Weka akili timamu           Kelele zisijezuke

Ujue na kufahamu           Kwa hayo na uridhike

Wengi wamejihujumu       Subiri watu wacheke

UPO !

Bushako umahashumu     Nadhari bora uweke

Tafakari  Muadhamu        Usiyarushe mateke

Kwaheri pendo lidumu      Tulia usisumbue

Ya KUONANA !

Huyo Babengwa Akupendae !!! hahahaa....

Mahaba huwa adhimu, mno yakikulekeya

Tena yanakuwa tamu, nyonda zikiendeleya

Mara yanakuwa sumu, siku yakikuzingiya

Tafakari muadhamu!

 

Nakuonavyo wasota, katwani humakiniki 

Wastahabu kutota, maneno huambiziki

Mahaba yaliyoota, ni shida hayakungoki

Nakuombea salama!

 

Mahaba hukuliwaza, kwa furaha ukawanda

Mwisho yajakutukiza, mwili wako ukakonda

Bushako nakueleza, usidhihaki na nyonda!

Nakunasihi Bushako!

 

Mahaba yana dharubu, Bushako uniamini

Yana mengi masaibu, si leo toka zamani 

Kwa pendo lilokuswibu, naomba uwe makini

Kwa heri ya kuonana!


Nduguyo: Swaleh Suheil Abeid (Sauti Ya Haki)

swalehe na babengwa ,   nyote  nawasikiliza

bushako hajawa bingwa, nasoma sitawabeza

nyumba ikawa  kungwa,    mukachoka kunisemeza

iki taka kula   chungwa ,     uchachu  utaumeza






bushako msema kweli ,  kusini na kaskazi

jambo kwake halifeliii,    ugumu wa kiangazi

kwa penzi amekubali,      hata kuwa mpagazi

kulikwepa ni  muhali,      nabembeleza mapenzi






  1. kuna wakati nakhisi,   nastahabu kila dhiki
  2. nishakula zake bisi ,    kwake niwe mstahiki
  3. nawauliza  waasisi,      mbona napata mashariti
  4. au kupenda mi najisi,   kujitoharisha nifanye vipi?

Sio kua ni sharuti, kukupa njema kauli

Kwa pendo lilozatiti, zakukumba idhilali

Bora mche Jabaruti, upate sitiri hali

Rakataini uswali!

 

Hebu mwepuke bilisi, pendo liwe la halali

Jiandalie harusi, suna ya wetu Rasuli

Heri uowe upesi, ukondoke mushikili

Nakuombea sahali !

 

Bushako sinilaumu, kukupa wangu ukweli

Ndoa kwako ni muhimu, takubariki Jalali

Ingawa mi si imamu, nakuombea sahali

Kaowe binti halali!

 

Nduguyo: Swaleh Suheil Abeid  'Sauri Ya Haki"

RSS

© 2012   Created by zanzibarwebsite.com.

Lebo  |  Report an Issue  |  Terms of Service