Nalia napokumbuka, ifikapo siku yangu
Udongo tanifunika, tita liwe juu yangu
Siweze tena kutoka, nibakie peke yangu
Hiyo ndio siku yangu, tapoiaga dunia!
Kifikiria mauti, hutetema moyo wangu
Na ufikapo wakati, tauaga ulimwengu
Takoma zangu kunuti, swalati na dua zangu
Tanitoka roho yangu, tapoiaga dunia!
Nitaiaga dunia, nitengeke na wezangu
Sina tachokichukua, ila ni amali yangu
Hesabu yaningojea, sijui mezani yangu
Una hofu moyo wangu, tapoiaga dunia!
Nyumba iliyo nyembamba, takua makao yangu
Kiza kitachonikumba, kimbele ya macho yangu
Siwezi tena kuomba, ningoje hukumu yangu
Hako mtetezi wangu, tapoiaga dunia!
Aridhi ndio tandiko, takua malazi yangu
Hakuna taekuwako, atulize khofu yangu
Kwa hayo misukosuko, tahimili peke yangu
Tabakia peke yangu, tapoiaga dunia!
Wote watanikimbia, swahiba na watu wangu
Udongo nitolalia, takua ni mto wangu
Maringo yashanishia, sina tena cheo yangu
Takwisha ubosi wangu, tapoiaga dunia!
Takuwapi wa murua?, chaguo la moyo wangu
Naye atanikimbia, aniwache peke yangu
Vya ajabu tanijia, viumbe vya bwana Mungu
Wenye ya moto marungu, wajapo kunihujia!
Ya Rabi nijaalia, nifuzu hesabu yangu
Siku hiyo kiwadia, usamehe dhambi zangu
Pepo yako niridhia, iwe masikani yangu
Uniweke kwenye fungu, la waja wako radhia
Tamati tuikumbuke, siku hiyo ya matungu
Bure tusipumbazike, kwa raha za ulimwengu
Dini yetu tuishike, tumogope Bwana Mungu
Una kicho moyo wangu, tapoiaga dunia!
SWALEH SUHEIL ABEID
'Sauti Ya Haki' Dubai - U.A.E.
Kurasa:
Bismilahi Rahimi Siku yenye ithibati
Kifo ni jambo azimi Isosomeka wakati
Si Suheli sio mimi Kaumu yetu umati
KUONJA KWETU MAUTI- ALLAH AMETANGAZIA.
Kilio hakisimami Unapofika wakati
Roho haijihami Yake Maluki Mauti
Yoyote hamsakami Nguvu zilojizatiti
KUONJA KWETU MAUTI- ALLAH AMETANGAZIA.
Ewe Mja Yailahi Uhai yako bahati
Kimbilia na kuwahi Tumia wako wakati
Tenda yenye maslahi Yamridhio 'Al- Muqsiti'
KUONJA KWETU MAUTI- ALLAH AMETANGAZIA.
Tafakuri Ya Mauti Hayataki hisabati
Jee, ushajizatiti Kuyakabili mauti ?
Fikiri na kusukuti Ufe ukawa hujuti
KUONJA KWETU MAUTI- ALLAH AMETANGAZIA.
Irabu niloiweka Sisitizo ya Umati
Bora ujumbe kufika Tusilie Yalaiti
Wajibu tukasikika Kuliko kuwasaliti
KUONJA KWETU MAUTI- ALLAH AMETANGAZIA.
Permalink Imejibiwa na Swaleh Suheil Abeid on January 24, 2012 at 11:16am Babengwa hujakasiri, kweli zako kalimati
Kusema kwa ujasiri, siku yenye ithibati
Wajibu kuifikiri, ziwe njema hisabati
Daima tuyakumbuke, Mauti yatungojea
Hebu tuwe na fahamu, tuombe kila wakati
Siku hiyo ikitimu, hayakingiki mauti
Ghafula tu marehemu, kinga njema hesabati
Daima tuyakumbuke, Mauti yatungojea
Wako wapi makhuluki, katika wetu umati?
Walokua ni Maliki, wakwasi wenye dhuriyati
Mara wakitahamaki, wameshazikwa tiati !
Daima tuyakumbuke, Mauti yatungojea
Permalink Imejibiwa na Dikupa on January 24, 2012 at 11:44am yaweza kuwa shirki, mja kuhofu mauti,
ambayo hayamfiki, ila muda na wakati,
saa atapo fariki,yumo kwenye harakati,
ameshika guruneti,
jihadi mwendo mtundo!
Amuitika munadi, wito kwenda jannati,
pale afapo shahidi, wallahi hiyo bahati!,
ameshika guruneti,
jihadi mwendo mdundo!
mara 'ti' 'parakacha', kalifyatuwa roketi,
hudumu bila kuwacha, hamsa yu swalawati,
anapo pambana kucha, roho yuko sakarati,
ameshika guruneti,
jihadi mwendo mdundo!
akipona "songa mbele!", anafata khutuwati,
hata kama kwa gobole, au jiwe la manati,
atapopigwa mshale, kuwa hoi, maututi,
ameshika guruneti,
jihadi mwendo mdundo!
ndipo huja malaika, kwa maelfu umati,
kuwa "ewe mtajika", nafsiyo mardhwati,
Peponi wahitajika, mafutuha lako geti,
una tele khairati,
leo furahi, uhondo!
Dikupa Dikupatile Dikilema (cheko lenye afya)
Permalink Imejibiwa na Swaleh Suheil Abeid on January 24, 2012 at 2:25pm Kufa kwako kwa jihadi, kuondoa dhulumati
Kwa kifo cha ushahidi, takujazi Jabaruti
Na ndio yake ahadi, una tele khairati
Utangia jan'nati, ufapo kwenye jihadi
Uwe safi wa fuadi, mwenye imani thabiti
Uwe kati ya junudi, ulipuwe guruneti
Uwe jasiri shadidi, usiogope mauti
Utangia jan'nati, ufapo kwenye jihadi
Sijifanye mujirimu, kuwalipua umati
Na kwajifunga mabomu, ufe kwa uafiriti
Ni kifo cha udhalimu, na thawabu huzipati!
Utangia jan'nati, ufapo kwenye jihadi
SWALEH SUHEIL ABEID 'Sauti Ya Haki'
© 2012 Created by zanzibarwebsite.com.